Friday, July 16, 2010

JK Kuvunja Bunge Leo

RAIS Jakaya Kikwete, leo jioni anatarajia kufunga na kulihutubia Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linamaliza muda wake Agosti mosi mwaka huu.

Hotuba ya Rais Kikwete ni ya mwisho kwa Bunge la 20, ambalo limepachikwa jina la Kasi na Viwango (Speed and Standard), chini ya uongozi wa Spika Samuel Sitta ambaye kwa kiasi kikubwa ameliongoza kwa mafaniko makubwa.

Maandalizi ya sherehe za ufungaji huo yameanza nje ya viwanja vya Bunge, ambapo askari wa Jeshi la Polisi walionekana wakifanya mazoezi kwa ajili ya kupamba ufungaji.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Job Ndugai, Rais Kikwete anatarajia kuingia kwenye viwanja vya Bunge majira ya saa 10 jioni.

Shamra shamra hizo, zitaendelea jioni ambapo kutakuwa na sherehe kubwa ya wabunge kuagana na kutakiana heri kwenye mikikimiki ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 31 mwaka huu.

Bunge la awamu ya nne litakumbukwa kwa hoja nyingi miongoni mwake ni ile ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, ambayo ilimfanya Waziri Mkuu Edward Lowassa ajiuzulu pamoja na mawaziri wengine Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashairiki).

Kujiuzulu kwa Lowassa kulilifanya Baraza la Mawaziri, livunjwe na kuundwa jingine huku, Mizengo Pinda akiteuliwa na kuidhinishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu.

Hoja nyingine itakayokumbukwa kwenye Bunge hili ni hoja ya wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), iliyotolewa na mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa (CHADEMA), ambaye hata hivyo alilazimika kuiondoa kutokana na upinzani mkali alioupata kutoka kwa wabunge wa chama tawala.

Hata hivyo, serikali ilijikuta ikilazimika kukubali uchunguzi dhidi ya akaunti hiyo ambayo baadaye ilibainika kiasi cha sh bilioni 133 kiliibwa na mpaka sasa baadhi ya watuhumiwa wa wizi huo kesi zao ziko mahakamani.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), hatolisahau Bunge hilo baada ya kufungiwa kwa madai ya kusema uongo dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini kwa wakati huo Nazir Karamagi kwa kusaini mkataba wa mgodi wa Buzwagi.

No comments:

Post a Comment