Wednesday, August 4, 2010

Ni Serikali ya Mseto Zanzibar.

SERIKALI ya umoja wa kitaifa (GNU) imeanza kunukia Zanzibar, baada ya serikali kuandaa marekebisho ya katiba yatakayowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Jumatatu ijayo.

Kwa mujibu wa marekebisho hayo ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambayo Tanzania Daima imepata nakala yake, Rais wa Zanzibar atatoka chama kilichoongoza katika uchaguzi, makamu wa kwanza atatoka chama cha upinzani kilichofuatia na kutakuwa na makamu wa pili wa rais ambaye atakuwa mtendaji mkuu serikalini atakayetoka chama tawala.

Ibara ya 39 (1) (2) ya mapendekezo hayo inasema rais ndani ya siku saba baada ya kushika madaraka atatakiwa kuteua makamu wa kwanza wa rais na makamu wa pili.

Hata hivyo, marekebisho hayo ya sheria yameeleza makamu wa kwanza wa rais atateuliwa na rais baada ya kushauriana na chama kilichopata nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar.

Tangu kuanza kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi Zanzibar chama cha CUF ndicho pekee kimekuwa kikipata viti vya uwakilishi na ubunge na kimekuwa kikitoa upinzani mkubwa kwa chama tawala CCM.

Mapendekezo hayo ya marekebisho ya katiba yanasema iwapo hakutakuwa na chama kilichofikisha asilimia tano ya kura za rais au rais kukosa mpinzani katika uchaguzi, nafasi ya makamu wa kwanza wa rais itapewa chama chochote cha upinzani kilichotokea nafasi ya pili kwa wingi wa majimbo.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo ibara ya 39 (1) (7), makamu wa pili wa rais ndiye atakuwa mshauri mkuu wa rais katika kutekeleza kazi zake na pia atakuwa ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hakutakuwa na Waziri Kiongozi.

Aidha, mapendekezo hayo yanasema rais atateua mawaziri kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuzingatia uwiano wa viti vya majimbo wa vyama vya siasa vilivyomo ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Kwa mujibu wa muswada huo, makamu wa kwanza wa rais hatakuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, isipokuwa atakuwa mshauri wa rais na atafanya kazi zote atakazopangiwa na rais.

Pia muswada huo unaeleza kuwa kutakuwa na makatibu wakuu katika Afisi ya Rais, makamu wa kwanza na makamu wa pili, ambapo wadhifa wa Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi umefutwa na badala yake kutakuwa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Kwa muswada huo, Katibu Mkuu Kiongozi ndiye atakuwa kiongozi mkuu wa watumishi wa umma Zanzibar.

Muswada huo wa sheria umebadilisha maneno ndani ya kifungu cha 37 (2) cha Katiba ya Zanzibar yanayohusu vitendo vya kudhalilisha Muungano na badala yake kuingiza maneno ‘mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais.’

Muswada huo pia umegusa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kikiwemo cha Kukomesha Magendo (KMKM), Jeshi la Kujenga Uchumi na Chuo cha Mafunzo, ambavyo baada ya kupitishwa muswada huo vitaitwa Idara Maalumu.

Muswada huo pia unampa uwezo Rais wa Zanzibar kuteua wakuu wa mikoa bila ya kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mikoa mitano ya Zanzibar.

Awali kifungu cha 61 kilikuwa kimeweka masharti kuwa Rais wa Zanzibar atateua wakuu wa mikoa kutoka kila mkoa kati ya mikoa mitano ya Zanzibar kwa kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Muswada wa marekebisho hayo ya Katiba ya Zanzibar umekuja siku tatu tangu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kutangaza matokeo ya kura ya maoni, ambapo wananchi wengi waliunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Khatib Mwinyichande, Jumapili iliyopita, wananchi wa Zanzibar kwa asilimia 66.4 waliunga mkono serikali hiyo kwa kupiga kura ya ndiyo, ambapo Kisiwa cha Pemba kimeongoza kwa kukubali mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Katika Kisiwa cha Unguja, majimbo manane kati ya majimbo 32 yalipiga kura ya kukataa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini majimbo yote 18 upande wa Pemba walipiga kura ya ndiyo.